Dodoma

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

MKUFUNZI wa sheria katika Shule Kuu ya Sheria Tanzania, Prof. Clement Mashamba, amesema kuwa Tanzania inashindwa kesi nyingi za uwekezaji kutokana na kutokuwa makini na kuvunja masharti ya uwekezaji huku akitaka mabadiliko ili kuepuka hasara kwa nchi.

Mwanasheria huyo ameyasema hayo hivi karibuni wakati akitoa mafunzo kwa waandishi na wahariri nchini yaliyoandaliwa na Muungano wa asasi za kiraia wanaofanya Uchambuzi wa Sera za Uwekezaji na Biashara (TATIC) kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa mikataba ya uwekezaji kimataifa (IIA).

https://www.youtube.com/watch?v=kLWitCJAAT0 

Ametoa mifano ya kesi  mbalimbali ambayo Tanzania imekua ikishtakiwa kwenye mahakama za kimataifa za usuluhishi ambazo inashindwa.

Prof. Mashamba ameeleza kuwa  kesi nyingi ambazo Tanzania imefunguliwa na kushindwa,imetokana nan chi kuvunja masharti ya sheria ya uwekezaji, na kwamba ni lazima yafanyike mabadiliko.

“Waatendaji hasa katika ngazi ya halmashauri wengi wao wamekuwa hawafahamu masharti yaliyomo kwenye hii mikataba kwa hiyo wanafanya maamuzi ambayo yanagusa haki za kulindwa za wawekezaji.

Kwa mujibu wa Prof Mashamba, wakati mwingine pia kumekua na mabadiliko ya kanuni mbalimbali mfano katika sheria ya madini iliyorekebishwa mwaka 2018 ilipelekea kufutwa leseni za utafutaji wa madini,leseni ambazo zilikuwa zinawapa kibali cha muda mrefu wawekezaji, leseni hizo zilifutwa bila kujali kwamba baadhi ya nchi wawekezaji wana mikataba ya kimataifa ya uwekezaji.

“Wawekezaji wanatakiwa kulindwa kwa namna mbalimbali, mojawapo ni isitungwe sheria inayoathiri uwekezaji wao,mfano wa kesi za aina hii ni kama ya hivi karibuni katika mradi wa Nikel wa Ntaka Hill.

Kesi hizi tulishindwa kwasababu ya hizo kanuni lakini pengine wanasheria wetu wangeweza kumshauri waziri husika wa madini waengeweza kutengeneza kifungu amabacho kingeweza kuepuka migigoro kama hiyo.”Prof Mashamba.

Julai mwaka huu, Tanzania ilitakiwa kulipa fidia ya dola milioni 109 (Sh. bilioni 260), kwa Kampuni ya Indiana Resourcesiliyoshinda kesi katika Mahakama ya Kimatiafa ya usiluhishi wa migogoro ya uwekezaji (ICSID), baada ya kuwepo ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji.

“Kesi nyingi hufunguliwa kutokana na matendo yetu, ni mara chache sana utakuta wawekezaji nao wamevunja mikataba, sababu nyingine inayopelekea kushindwa kesi za aina hii  ni kutokana na kukosa ushahidi, tukifunguliwa kesi, wanasheria wetu wanakosa hoja nzuri za utetezi.

Kwa mujibu wa Profesa Mashamba, waandishi wa habari wanatakiwa kufahamu kwa kina umuhimu wa sheria za kimataifa za uwekezaji kwa manufaa ya nchi yetu, ili waweze kuripoti kwa namna itakayosaidia jamii.

 

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TATIC, Olivia Costa amesema ni muhimu kwa wanahabari kupata maarifa na ujuzi wa mikataba ya uwekezaji kimataifa, ili watoe taarifa kuhusu makubaliano mbalimbali kwa ufanisi mzuri.

 

Amesema mafunzo haya yameundwa kutoa ujuzi wa kutosha kwa waandishi wa habari na kutoa taarifa kwa umma kuhusu jukumu muhimu la IIA katika kuunda uchumi wa dunia.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, habari mbalimbali zitakazochapishwa na kutangazwa zitachangia kufanya mazingira ya uwekezaji kuwa wazi zaidi na kuimarisha ukuaji endelevu na maendeleo kwa Tanzania, kwa manufaa ya wote.

 

“Katika siku hizi mbili, waandishi wa habari watafahamu  historia na mabadiliko ya Mikataba ya Uwekezaji ya Kimataifa (IIA), vipengele muhimu na malengo yake, na athari zake kwa wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na serikali, wawekezaji,wananchi na maendeleo ya nchi,”amesema Oliva na kuongeza:

 

“Pia Waandishi watajifunza kuhusu changamoto na fursa zinazohusiana na IIA na jinsi mwenendo wa sasa katika sheria na uchumi wa kimataifa unavyoziunda.”

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliwashukuru TATIC huku wakieleza kuwa watakwenda kutumia vyema kalamu zao kuelimisha umma kupitia kuandika habari, kutengeneza vipindi na kualika wageni kwenye vyumba vya habari ili wananchi wawe na uelewa mkubwa.