Ateua Waziri, Makatibu Wakuu, Manaibu na Wakuu wa taasisi
Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

RAIS Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya nne ya Baraza la Mawaziri tangu aingie madarakani Machi 19, mwaka 2021, huku akihamisha wengine huku akiteua Makatibu Wakuu wapya tisa, kuhamisha watano na Manaibu Katibu Mkuu wapya 11 na Mkuu wa Mkoa mpya mmoja.

Uteuzi huo umefanyika leo (Februari 26,2023) na viongozi hao wataapishwa Februari 27, mwaka huu saa 10:00 jioni katika Ikulu ya Chamwino Dodoma.

Katika uteuzi uliofanyika jana, maofisa wanne wa Ofisi ya Rais, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Meneja wa NEMC Kanda ya Kati, wameteuliwa kuwa Manaibu Katibu Mkuu.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Februari 26, 2023 na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Moses Kusiluka, Rais Samia amemteua Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo akichukua nafasi ya Pauline Gekul aliyehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria.

Aidha, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abadallah Ulega, ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi akichukua nafasi ya bosi wake Mashimba Ndaki ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

 

Abdallah Ulega

Hamis Mwijuma

WALIOHAMISHWA

Aidha, Rais Samia amewahamisha Wizara Naibu Mawaziri Gekul anayekwenda kuwa Naibu Waziri Katiba na Sheria huku Godfrey Pinda aliyekuwa Naibu Wizara Wizara ya Katiba na Sheria akienda kuwa Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Pauline Gekul

Geofrey Pinda 

Pia Ridhiwani Kikwete aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amepelekwa kuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora huku Deogratius Ndejembi akihamishwa kutoka Wizara hiyo kwenda kuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Ridhiwani Kikwete 

Deogratius Ndejembi

Aidha, David Silinde anatoka Wizara ya TAMISEMI anakwenda kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

David Silinde

WAKUU WA MIKOA

Rais Samia pia amemteuwa Christina Mndeme kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, akichukua nafasi ya Sophia Mjema aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi-Itikadi na Uenezi.

Vilevile, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Fransis Michael ameteuliwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe huku aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo akipelekwa mkoani Tanga kuchukua nafasi ya Omary Mgumba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

MAKATIBU WAKUU WAPYA

Rais Samia ameteua makatibu wakuu wapya na wizara zao kwenye mabano; Dk. Tausi Kida (Ofisi ya Rais Uwekezaji), Juma Mkomi (Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) na Balozi Samweli Shelukindo (Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki).

Wengine ni Prof. Carolyne Nombo (Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia), Gerald Mweli (Wizara ya Kilimo), Dk. Seif Shekalaghe (Wizara ya Afya), Nadhifa Kemikimba (Wizara ya Maji), Kheri Mahimbali (Wizara ya Madini) na Mohamed Abdulla Khamis (Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari).

WALIBADILISHWA WIZARA

Rais Samia pia amewabadilisha wizara makatibu wakuu watano ambao ni Prof. Riziki Shemdoe aliyetoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwenda Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. John Jingu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) kwenda Wizaya ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Dk. John Jingu

Wengine ni Dk. Jim Yonazi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), huku Adolf Ndunguru akitoka Wizara ya Madini kwenda Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Anthony Sanga ametoka Wizara ya Maji kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

MANAIBU KATIBU WAKUU WAPYA

Katika uteuzi huo Rais Samia pia ameteua manaibu makatibu wakuu wapya, akimteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Wilson Mahera kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI (Afya).

Wilson Mahera

Pia amemteua aliyekuwa Ofisa Mwandamizi Ofisi ya Rais Ikulu, Sospeter Mtwale kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, huku aliyekuwa Meneja wa NEMC Kanda ya Kati, Dk. Franklin Rwezimula akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekonolojia (Elimu ya Msingi na Sekondari).

Rais Samia pia amemteua Ofisa Mwandamizi Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Hussein Omari kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo huku aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Cyprian Luhemeja akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji.

Cyprian Luhemeja

Pia aliyekuwa Mkurugenzi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Lucy Kabyemera, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wizarani humo, huku aliyekuwa Ofisa Mwandamizi Ofisi ya Rais Ikulu, Andrson Mutatebwa, akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasilia na Utalii.

Rais Samia amemteua aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Athuman Mbuttuka, kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati huku akimteua Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania, Dk. Daniel Mushi, kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Pia amemteua aliyekuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Agnes Meena, kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi huku aliyekuwa Ofisa Mwandamizi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Selestine Kakele, akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

MANAIBU WALIOHAMISHWA

Katika uteuzi huo, Manaibu Makatibu Wakuu wawili wamehamishwa wizara ambao ni Dk. Grace Maghembe aliyekuwa TAMISEMI sasa anakwenda Wizara ya Afya na Nicholas Mkapa aliyekuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

NEC

Rais Samia pia amemteua Ramadhani Kailima kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi akichukua nafasi ya Mahera aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu - TAMISEMI.

Haya ni mabadiliko ya nne tangu Rais Samia aingie madarakani na kuwa Rais wa Awamu ya Sita baada ya Aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli kufariki dunia.

Aidha, mabadiliko ya hivi karibuni yalifanyika Februari 14, 2023 na kuzigusa Wizara ya Maliasili na Utalii na Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ikiwa ni siku 12 zilizopita.

Desemba 8, mwaka 2022 akihutubia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia aliomba ridhaa ya kupanga upya serikali yake ili kuwa na viongozi watakaoendana na kasi yake, na siku chache baadaye alifanya mabadiliko Wizara ya Maliasili na Utalii.