Na Salome Kitomari
Dar es Salaam, Tanzania

BALOZI wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Ami Inbar ameeleza nia yake ya kuendelea kusaidia familia duni na jamii za wafugaji kubadili maisha yao kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao, balozi huyo ambaye anafahamika kwa kuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Milenia (SDG), alisema matamanio yake ni kuona watu wa familia duni, maisha yao yanabadilika.

Balozi Inbar ambaye ni mwanzilishi wa mfuko wa kusaidia jamii wa Nau Charitable Fund na mwenye mchango mkubwa kwenye kulinda utambulisho wa pekee wa nchi, alisema mara zote alipokuwa Tanzania ameshirikiana na jamii za wafugaji ya Maasai kwenye shughuli za uzalishaji.

Amesema kutokana na kazi hizo ameshirikiana na taasisi nyingine kama Marvelous Foundation ya New York, Marekani na pia amefika nchi za Ukraine, Israeli, Ugiriki na Dubai. Taasisi hiyo inatekeleza miradi mbalimbali ya kuwezesha jamii nchi za Tanzania na Kenya kupata chakula, elimu na huduma za afya kwa watoto wenye uhitaji na watu wazima.

Amesema kuwa yeye na wenzake wanawasaidia watoto kutoka familia za mzazi mmoja kupata mahitaji yote ya elimu ikiwamo kulipa ada katika Shule ya O’Brien iliyoko katikati ya Moshi na Arusha ambayo ni kwa ajili ya watoto wa jamii ya kimasai.

Balozi Inbar akiwa na mifugo huko Manyara.

“Kutokana na msaada wetu tumerudisha tabasamu kwa watoto hawa ambao sasa wanaendeleo na masomo, wanatoka familia duni ambazo ni za mzazi mmoja na walikuwa nyumbani kwa sababu walikosa ada.

“Ni muhimu sana kuwapa elimu kwa ajili ya maisha yao ya baadaye, shuleni wanapewa sare za shule, viatu na chakula. Lakini walikosa ada, hivyo tumewawezesha kuendelea na masomo bila kikwazo chochote,” amesema.

Kwa mujibu wa Inbar, alihamaisha wenzake ambao walikwenda mkoani Arusha na kukutana na jamii ya kimasai ambao waliwaeleza changamoto zao ni ukosefu wa maji, chakula, dawa na huduma za mifugo.

 

“Tumepeleka misaada muhimu kama dawa, chakula, vinywaji na tumenunua ng’ombe 200 wakati huo na tuna mpango kuongeza ili kuwawezesha kupata maziwa na mazao mengineyo ya mifugo. Kwa kweli tulikutana na wahitaji wengi sana,"amesema.